Saturday, December 12, 2015

Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova Dar es Salaam. Moto aliouwasha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kubaini upotevu mkubwa wa makontena na kuikosesha Serikali mapato umeendelea baada ya maofisa 40 wa mamlaka mbalimbali za umma kukamatwa na kurejeshwa kwa Sh10 bilioni zilizopotea kwa ukwepaji kodi. Jana, Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam ilitangaza kuwashikilia maofisa hao kwa tuhuma za kula njama za kutorosha makontena 329 kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kuikosesha Serikali mapato. Kati ya watuhumiwa hao, polisi ilieleza kuwa 26 ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), 11 ni wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na watatu ni watumishi wa Bandari Kavu (ICD) inayomilika na Kampuni ya Azam. Kamishna wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema kuwa watuhumiwa hao ni wapya wanahojiwa kuhusiana na tuhuma hizo ili kubaini wahusika zaidi wa mtandao wa ukwepaji kodi huo. “Uchunguzi utakapokamilika jalada lao litapelekwa kwa Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi. Sisi (polisi) hatuna mzaha katika suala hili, tutahakikisha watuhumiwa wengine zaidi waliohusika kwenye kashfa hii wanakamatwa,” alisema Kova. Alisema uchunguzi unaofanywa na polisi, pia unahusisha kupitia kumbumbuku mbalimbali na kadhia za forodha ili kubaini mtindo uliotumika katika mchakato huo, Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika na makontena 2,489 yalitolewa bila ya kulipiwa kodi. Kova alisema makontena 329 yaligundulika kupotea kwenye bandari kavu ya Azam kati ya Julai hadi Novemba mwaka huu. Aidha, makontena 2,489 yalitolewa Bandari ya Dar es Salaam kati ya Machi hadi Septemba 2014, kinyume cha taratibu kwa lengo la kukwepa kodi na ushuru. Wakati huohuo, Kamishna Kova alisema polisi inamtafuta mtu aliyemtaja kwa jina la Abdulkadir Kassim, mkazi wa Temeke, Dar es Salaam ambaye pia ni wakala wa forodha wa Kampuni wa Regional Cargo Sevrvice LTD, aliyedai kuwa kinara wa kutoa makontena 329 kwenye ICD ya Azam. Alisema kuwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwake au kutoa taarifa za kukamatwa kwake, atazawadiwa Sh20 milioni na kwamba endapo yupo jijini ajisalimishe. “Tumewakamata wenzake wawili, tunafanya mahojiano nao, ila yeye (kinara) inasemakana amekimbia, namuomba ajisalimishe,” alisema Kova. Mbali ya harakati za Majaliwa aliyefanya ziara bandarini na kufanya ukaguzi wa kushtukiza, Rais John Magufuli aliwapa siku saba wafanyabiashara waliokwepa kulipa ushuru , kulipa kabla ya Serikali haijawachukulia hatua. Meneja wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Diana Masala alisema hadi juzi , kampuni 22 zilizodaiwa kukwepa kulipa kodi katika makontena hayo zililipa Sh10 bilioni. Alifafanua kwamba makontena 329 yalikuwa na thamani ya Sh28 bilioni, lakini kiasi sahihi cha kodi kilichotakiwa kulipwa TRA ni Sh 12 bilioni. Hivyo, hadi sasa bado Sh2 bilioni hazijarejeshwa kama kodi ya Serikali. “Tunaomba kampuni ambazo hazijalipa, kulipa mara moja kama wenzao walivyofanya. Leo ndiyo siku ya mwisho kama alivyoagiza Rais (Magufuli), kama hawajitokeza hatua zaidi za kisheria zitafuata,” alisema Masalla Aliongeza kuwa TRA, itatoa zawadi nono ya asilimia 3 ya kodi iliyokombolewa ambayo haizidi Sh20 milioni kwa mtu au watu watakaofanikisha kukamatwa kwa mtu au kampuni inayokwepa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

le=1">