Wednesday, March 30, 2016

Japan yaikopesha Tanzania Bil 117

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati mbili za
makubaliano na Serikali ya Japan itakayoiwezesha Tanzania kupata
kiasi Yen Bilioni 6 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 117 za Kitanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini hati
hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius
Likwelile alisema mkataba wa kwanza utasaidia katika kukamilisha
bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17.
Dkt. Likwelile alisema kuwa msaada huo unalenga kuweka
mazingira rafiki kwa wafanyabiashara, kuboresha masoko na
kuwezesha mazingira ya ushindani katika utengenezaji wa ajira
nchini.
Mkataba wa pili unahusu masuala ya kiufundi yatakayotumika
katika kufanya marekebisho ya mkataba uliosainiwa Octoba 20,
1966, kwa kuzingatia sheria nyingi zimebadilika, kusainiwa kwa hati
hiyo ya makubaliano itasaidia kutabadilisha baadhi ya vifungu
vyenye jina Tanzania na kuweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ili kujumuisha pande zote mbili za Muungano katika kutekeleza
miradi ya maendeleo nchini.
Aidha, makubaliano hayo yatasaidia kubadilisha baadhi ya vipengele
vya mkataba uliopita ikiwemo kipengele cha usambazaji wa
madawa ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa ya wataalamu kutoka
nchini Japan kuweza kuja kufanya kazi za kujitolea hapa nchini
Tanzania.
Katibu Mkuu Dkt. Likwelile ameishukuru Serikali ya Japan na
kusisitiza kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa ili kuweza
kuwa na tija na kuwaletea maendeleo Watanzania.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida
amesema kuwa Serikali ya Japan ina imani kuwa ushirikiano uliopo
baina ya nchi hizi mbili utasaidia kukuza maendeleo ya uchumi na
kijamii.
Balozi Yoshida amesema kuwa Serikali ya Japani inaunga mkono
juhudi za Serikali inayo ongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika
masuala ya viwanda na mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji
kuwekeza nchini Tanzania.

Raia wa Japan ajinyonga Tabora

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mtu mmoja Raia wa Japan aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya Konoike
inayoshughulika na mradi wa maji vijijini,amekutwa amejinyonga katika chumba cha kufanyia uchunguzi wa
udongo,bila kuacha ujumbe wowote.
Tukio hilo limeibua mshangao kwa wananchi wa Tabora na wafanyakazi wenzake.
Akidhibitisha tukio hilo,Kamanda wa Polisi mkoani Tabora Kamishina Msaidizi Hamis Suleiman,amemtaja
marehemu kwa jina la Akihila Takahashi(49),akidai kuwa tukio hilo ni la kushangaza,na ni la kwanza mkoani
Tabora mtaalamu na Raia wa Kigeni kujinyonga,huku akisema kuwa uchunguzi wa kina unafanyika.
Wafanyakazi wenzake wamesema kuwa,jana yake walikuwa naye kazini kama kawaida.
ITV

Gary Neville atimuliwa Valencia

Gary Neville ametimuliwa kuifundisha klabu ya Valencia inayoshiriki
ligi kuu ya Hispania, La Liga baada ya siku 120.
Neville mlinzi wa zamani wa Manchester United ameiongoza
Valencia kwenye michezo 28 akifanikiwa kuibuka na ushindi katika
michezo 10 pekee.
Mwenyewe amekubali licha ya kuwa alitamani kuendelea
kuifundisha Valencia lakini ameshindwa kufikia matarajio ya klabu

WATUMISHI HEWA 2,620 WABAINIKA, RIPOTI NZIMA YA MIKOA 23 IKO HAPA

Na Martha Magawa, Moshi Shabani
HATIMAYE wakuu wa Mikoa yote nchini wametii agizo la
Rais John Magufuli lilokuwa linawataka wasilishe ripoti ya
idadi ya watumishi hewa kwenye mikoa husika.
Wakuu hao wa mikoa wapya wamewasilisha ripoti za
watumishi hao leo Jijini Dar es Salaam,Waziri wa
Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa,Georgy Simbachawene ili kuchukuliwa hatua za
kisheria kwa watumishi waliohusika katika kashfa hizo,
Mkoa wa Dar Es Salaam .
Akiwasilisha ripoti ya watumishi hewa.Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda amesema katika mkoa wake
baada ya kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na kamati
mbali mbali wamebaini kuwepo kwa watumishi hewa 73
ambao watumishi hao hewa wamepelekea serikali kupotea
pesa zaidi ya Milioni 316 kwa mwaka mmoja.
“Katika mkoa huu tumepata watumioshi hewa 73,ila wengi
watahoji mkoa huu mkubwa kwanini unakuwa na
watumishi hewa wachache,nakata kukwambia Waziri, bado
tunaendelea na uchunguzi wa kina”amesema Makonda .
Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Daudi Felix
Ntibenda amesema katika mkoa huo umegundurika kuwepo
na watumishi hewa 270 ambao wamekuwa
wakiisababishia hasara serikali ya Bilioni 1.8 kwa kipindi
cha Mwaka mmoja,
Mkoa wa Dodoma.
Pia Mkuu wa Dodoma Jordan Lugimbana amesema katika
mkoa wake wamegundua kwenye mkoa huo kuna
watumishi hewa 101 ambao amedai wameisabishia hasara
serikali Milioni 287.3 kwa kipindi cha miezi sita.
Mkoa wa Iringa.
Mkoa wa Iringa Amina Masenza amesema katika mkoa
wake wamegundua kuwa kuna watumishi hewa 15 ambapo
amemweleza Waziri Simbachawene kuwa licha hao kuna
watumishi 145 ambao hajaonana nao huku akidai kuwa
akimaliza kuonana nao huwenda idadi ya watumishi hewa
ikaongezeka.
Mkoa wa Kagera .
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenelal Mstaafu Salum
Kijuu amesema mkoa wake wamebaini kuwepo kwa
watumishi hewa 14 ambao wamesababisha upotevu wa
pesa za serikali Milioni 49.1
Mkoa wa Katavi,
Pia Mkuu wa mkoa huu, Jeneral Raphael Muhuga
amesema mkuo huo umegundurika kuwepo kwa watumishi
hewa 21 ambao wameitia hasara serikali Milioni 20.7.
Mkoa wa Kigoma .
Pia Mkoa wa Mkuo huyo, Bregedia Jenaral Mstaafu
Emmanuel Maganga amesema katika mkuo huo wamebaini
kuwepo watumishi hewa 171 ambao wameitia hasara
serikali milioni 114.6.
Mkoa wa Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa huo,Merck Sadick amesema wamebaini
mkuo wake umegundurika kuwepo na watumishi hewa 111
ambao wamekuisababishia hasara serikali hasara ya
milini 281.4.
Mkoa wa Lindi
Kwa Upande wa Mkuu wa mkoa huo,Godfrey Zambi
amesema mkoa wake unawatumishi hewa 57 ambao
wameitia hasara serikali milini 36.2.
Mkoa wa Manyara.
Kwa Upande wake mkuu wa mkoa huo,Joel Bendera,
amesema mkuo umekuwa na watumishi hewa 42 ambao
wameitia hasara serikali Milioni milioni 313.9.
Mkoa wa Mara .
Kuhusu Mkuoa wa Mara,Mkuu wa mkoa huo,Magesa
Mulongo amesema katika mkoa wake wamebaini kuna
watumishi hewa 94 ambao wameitia hasara serikali
milioni 121.
Mkuo wa Mbeya.
Kwa upande wa Mkoa wa Mbeya,Mkuu wa Mkuo huo,Amos
Makalla amesema katika mkoa wake kumekuwa na
watumishi hewa 98 ambao pia wameitia hasara serikali
Milioni 459 .6.
Mkoa wa Morogoro.
Hata hivyo mkuu wa mkoa huo,Dkt Steven Kebwe,ambapo
amesema mkoa wake umegundurika kuwepo na watumishi
hewa 122 ambao wameitia hasara serikali milioni 450.7.
Mkoa wa Mtwara.
Mkuu wa mkoa huo,Halima Dendegu amesema mkoa wake
ubainikika kuwepo kwa watumishi hewa 17, huku
watumishi wengine 285 uchunguzi ukiendelea,ambapo
watumishi hao 17 wameitia hasara serikali milioni 216.5.
Mkoa wa Mwanza .
Mkuu wa Mkoa wa John Mongella amesema mkoa wake
umengundurika kuwepo kwa watumishi hewa 334.
Mkoa wa Njombe .
Mkuu wa Mkoa wa NJombe,Dkt Rehema Nchimbi
amesema mkoa wake umekuwa na watumiwa na hewa 34
ambao amedai wamekuwa wakiitia hasara serikali Milioni
20.1.
Mkoa wa Pwani .
Mkuu wa Mkoa huyo,Mhandisi Evarist Ndikilo amesema
Mkoa wake umekuwa na watumishi hewa 150 huku
hakishindwa kusema hasara ya fedha za serikali kwa
madai kuwa uchunguzi unaendelea.
Mkua wa Rukwa .
Mkuu wa mkoa huo,Kamishna Mstaafu Zerote Steven
amesema mkoa wake umekuwa na watumishi hewa, 18 na
wametia hasara serikali milioni 55.6.
Mkuo wa Ruvuma ,
Mkuu wa Mkoa huo,Thabiti Mwambungu amesema mkoa
huo umekuwa na watumishi hewa 35 ambao wameitia
hasara serikali milioni 58.4.
Mkoa wa Simiyu .
Mkuu wa Mkoa huo,Antony Mataka amesema mkoa huo
umegundurika watumishi hewa 62 wameitia hasara
serikali ya Milioni 320.9.
Mkoa wa Singida ,
Mkuu wa mkoa wa huo,Mhandisi Methew Mtigumwe
amesema kuwa wafanyakazi hewa katika mkoa wake,231
nakueleza kuwa uchunguzi bado unaendelea ili kubaini
zaidi.
Mkoa wa Tabora
Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameanisha kuwa
katika mkoa wake watumishi hewa 48 ambapo wanaitia
hasara Serikali Milioni 118.7.
Mkoa wa Tanga .
Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela amesema kuwa
watumishi hewa katika mkoa wake ni 104 ambapo
amesema kuwa tathimini ya kuhakiki bado inaendelea.
Hata hivyo katika mkoa wa Shinyanga imekuwa tofautina
mikoa mingine ambapo hadi sasa hakuna watumishi hewa
kutokana na mikakati iliyowekwa na kuanzia Mwezi Julai
mwaka 2014 na mkuu wa mkoa aliyepita.

Messi awakera wa Misri

Mwanasoka bora duniani Lionel Messi amegawa viatu vyake vya
kusakata soka katika mnada wa hisani nchini Misri,bila kujua
kwamba hatua hiyo huenda ikawakera wengine.
Kisa hicho kinajiri wiki chache baada ya Messi kupongezwa kwa
kutimiza ndoto ya kijana mmoja wa Afghanistan alipomtumia mpira
na jezi yake.
Lakini mchezaji huyo alipoonyesha hisani kama hiyo huko Misri
katika runinga moja ya Misri wiki hii hatua hiyo lionekana na wengi
kuwa matusi .
Wakati wa mahojiano ya runingani katika kipindi cha Yes am
Famous kinachorushwa hewani na runinga ya MBC Misri,mchezaji
huyo wa Argentina aliwaambia watangazaji hao kwamba angependa
kutoa viatu vyake vifanyiwe mnada.
Kile ambacho Messi hakuelewa ni kwamba nchini Misri na mataifa
mengine ya Uarabuni viatu hutumika kama ishara ya kukosa
heshima ama hata matusi.
Hivyo basi raia wa taifa hilo walichukulia kitendo hicho kama
makosa na kuanza kutoa hisia kali katika mitandao ya kijamii.

Serikali yaombwa kutoa vibali vya Sukari

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo,Uvuvi na Maji imeiomba serikali kutoa vibali vya wafanyabishara ili kuingiza sukari ya nje kwa kipindi cha miezi mitatu ili kuondoa upungufu wa sukari uliopo.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Mary Nagu amesema kwa sasa nchi inakabiliwa na upungufu wa kati tani 80,000 hadi laki moja katika kipindi hicho ambacho kitakua ni cha matengenezo ya viwanda.

Dkt. Nagu amesema kuwa kwa kipindi ambacho miwa mingi inakua na maji hivyo inakua haifai kuzalisha sukari na ndicho hutumiwa na wazalishaji kufanya matengenezo ya viwanda vyao.

Aidha Dkt. Nagu amesema Machi 24 mwaka huu, kamati hiyo ilikutana na bodi ya sukari nchini na kuzungumza nayo ili kujua shughuli zao zinavyokwenda pamoja na changamoto zinazowakabili.

Aidha mwenyekiti huyo wa kamati amesisitiza kuwa vibali vinavyotakiwa kutolewa kwa wafanyabishara vinatakiwa kutumiwa vizuri kwa kufuata sheria na utaratibu wa serikali na sio kutumia mwanya huo kuingiza sukari nyingi itakayokuja kukutana na ya wazalishaji wa ndani.

CUF wakutana Zanzibar

Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama Cha Wananchi (CUF) leo
imeanza kikao chake cha siku mbili mjini Zanzibar chini ya Katibu
Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa, Kikao hicho kitaandaa ajenda
kwa ajili ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama litakalokutana
kwa siku mbili tarehe 2 - 3 April, 2016.
Baraza Kuu la Uongozi CUF linatarajiwa kutoa mwelekeo wa chama
hicho kuhusiana na hali ya kisiasa Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa ujumla.
CUF inakutana kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi
wa marudio visiwani Zanzibar Machi 20 ambapo chama hicho
kiliususia.
Chama cha Mapinduzi(CCM) kilizoa majimbo yote ya uchaguzi
Visiwani humo huku Dk Ali Mohammed Shein akishinda kiti cha
urais kwa kupata zaidi ya asilimia 91 ya kura zote halali.

Tuesday, March 29, 2016

Uchaguzi wa Zanzibar waikosesha hela Tanzania

Shirika la ufadhili la serikali ya Marekani limesitisha msaada wake
kwa serikali ya Tanzania likilalamikia matukio kuhusu uchaguzi wa
Zanzibar na kutekelezwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) imesema Tanzania
haijatimiza viwango vinavyohitajika ili kunufaika na ufadhili kutoka
kwa shirika hilo, na hivyo basi haitapokea msaada wa awamu ya pili
ambao ulikuwa wa jumla ya Dola 472.8 milioni ambazo ni sawa na
shilingi trilioni moja za Tanzania.
Kupitia taarifa, bodi hiyo imesema: "Serikali ya Tanzania
haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa
kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa Sheria ya
Uhalifu wa Mtandao.”
Bodi hiyo aidha imesema Tanzania iliendelea na uchaguzi wa
marudio Zanzibar ambao "haukushirikisha wote na wala haukuakisi
maoni ya wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani
na jamii ya kimataifa.”
Mabalozi wakosoa uchaguzi wa Zanzibar
Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt Ali
Mohammed Shein alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo uliosusiwa
na chama kikuu cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF).
MCC imesema kwamba huwa inatilia mkazo sana demokrasia na
kujitolea kwa nchi kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.
"Uchaguzi uliofanyika Zanzibar na kutekelezwa nwa Sheria ya
Uhalifu wa Mitandao vinaenda kinyume na hili,” imesema.
Tanzania ilipokea Dola 698 milioni katika awamu ya kwanza.
Pesa za MCC hutumiwa kufadhili miradi ya maji, barabara na
nishati.

Mwanamume aliyeteka ndege ya Misri akamatwa

Mwanamume aliyeteka nyara ndege ya shirika la Misri la EgyptAir
na kuishurutisha kutua Cyprus amekamatwa, wizara ya mashauri ya
kigeni ya Cyprus imetangaza.
Mwanamume huyo alidai kwamba alikuwa na mkanda wa kujilipua
na kumwamuru rubani wa ndege hiyo kuielekeza Cyprus au Uturuki.
Ndege hiyo, iliyokuwa safarini kutoka Alexandria hadi mjini Cairo,
mwishowe ilitua uwanja wa Larnaca nchini Cyprus.
Abiria karibu wote walikuwa wamefanikiwa kuondoka kutoka
kwenye ndege hiyo.
Ripoti zinasema kuwa mtekaji wa ndege ya EgyptAir anataka
kuongea na mkewe walietengana naye anayeishi Cyprus ambaye
kwa sasa anadaiwa kuelekea katika uwanja huo wa ndege.
EgyptAir: Mtekaji ataka kumuona ''mkewe''
Rais wa Cyprus Nicos Anastasiades amewaambia waandishi wa
habari kwamba tukio hilo la utekaji nyara halikuwa la kigaidi.
Akijibu maswali ya waandishi iwapo mtekaji huyo alishinikizwa na
mapenzi, alicheka na kusema, ''kila mara kuna mwanamke
anayehusishwa''.
Shirika la habari la Cyprus CYBC linasema kuwa mtekaji huyo
huenda alikuwa na malengo yake ya kibinafsi, mtekaji huyo alikuwa
na mkewe waliyetengana nchini Cyprus.
Walioshuhudia wanasema kuwa mtekaji huyo alirusha barua katika
uwanja huo wa ndege ilioandikwa Kiarabu akiomba ipelekwe kwa
mwanamke huyo.

Uchambuzi wa Humphrey Polepole Kuhusu Marekani Kusitisha Msaada wa Mabilioni ya Pesa na Shughuli zake Tanzania

Nianze na nukuu hizi mbili kuntu za Baba wa Taifa Mwalimu Julius
K. Nyerere- Mwenyezi Mungu amrehemu.
“Democracy is not a bottle of Coca-Cola which you can import.
Democracy should develop according to that particular country”.
June 1991 in Rio De Janeiro, Brazil
"Demokrasia sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza.
Demokrasia lazima ikue na kuendelezwa kulingana na nchi husika".
Juni 1991 Rio De Janeiro, Brazil (Tafsiri ni yangu)
“No nation has the right to make decisions for another nation; no
people for another people”. From ‘A Peaceful New Year’ speech,
Tanzania, January 1968
"Hakuna Taifa lina haki ya kufanya maamuzi juu ya Taifa lingine;
wala watu juu ya watu wengine ". Hotuba ya Amani ya Mwaka
Mpya, Tanzania, Januari 1968 (Tafsiri ni yangu)
Hili la Marekani na uamuzi wa MCC ni jambo la mpito na haliwezi
kuua mahusiano yetu na Marekani. Tanzania na Marekani
zinashirikiana kwa mambo mengi na MCC ni sehemu tu tena ni
eneo jipya la ushirikiano.
Uamuzi huu ni jaribio kwa uhuru wa Taifa letu. Hakuna namna
nyingine ila kushinda hili kama tulivyoshinda mengine huko nyuma.
Kwa wale ambao wameuona umri watakumbuka namna tulivunja
uhusiano na Ujerumani Magharibi 1964 pale walipotaka kuwa na
kauli hasi dhidi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Tulivunja uhusiano na Ujerumani Magharibi baada ya kutaka
kuingilia Uhuru wa Mataifa Mawili huru yaliyoamua kuungana na
kuunda Nchi Mpya ambayo leo tunajivunia, Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
1965 Tulivunja uhusiano na Uingereza kufuatia na kitendo cha
wazungu wachache kujitangazia Uhuru (Unilateral Declaration of
Independence) kule Rhodesia na uingereza kukaa kimya na
kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Tulivunja Uhusiano na Uingereza kuieleza Dunia kwamba Uhuru wa
nchi za Afrika ni kipaumbele muhimu kwa Tanzania. Jambo
tunalopaswa kufahamu ni kuwa MCC 2 toka mwanzo imekuwa ni
mtihani dhidi ya uhuru wetu.
Napenda ieleweke kwamba kipindi hiki kilichotokea sio kuvunjika
kwa uhusiano wetu na Marekani bali taasisi ya MCC ndio imesitisha
msaada wao kwetu, lakini mahusiano yetu na marekani bado yako
pale pale, na si Marekani au Tanzania inayoweza kuugharimu
uhusiano wetu.
MCC 1 ilikuwa ni chambo cha kutuvuta na tulipewa bila masharti
tena hela nyingi dola milioni 698 na ni fedha tulizopewa moja kwa
moja na kupewa uhuru wa kuamua tuzitumieje.
Tanzania ilitakiwa kuainisha maeneo kisha wao wanatoa hela. Ndio
maana miradi kama ile barabara ambazo hazikuwa zikipata ufadhili
kwa kuwa hazikuonekana ni za kiuchumi na miradi ya maji ya
Morogoro na kwingineko iliingizwa humu na kupata ufadhili.
MCC 2 sio hivyo. Kwenye MCC 2 walengwa wakubwa ni sekta
binafsi ya Marekani, hapa kuna mtego hapa, hapa ni biashara hapa.
Mchakato wa MCC 2 ulipoanzishwa, wafanyabiashara kwa
kushirikiana na Maseneta wakaanzisha hoja kuwa kwanini
Marekani inatoa fedha kwa ufadhili katika nchi ambazo China ndio
wenye kufaidika na fedha hizo?
Wakaleta hoja ya kuwa Serikali ya Marekani ifanye jitihada ya
kuweka fedha kwa kusaidia Sekta Binafsi ya Marekani kupenya
Afrika.
Ukaitishwa mkutano wa US-Africa Summit na agenda kubwa ikawa
Power Africa. Katika Power Africa, Marekani ikalichagua eneo la
Nishati (si uzalishaji viwanda) kwa kutambua kuwa ndio eneo
pekee wanaloweza kushindana na wachina.
Wakasema wataelekeza fedha huko kuisaidia Afrika kutatua tatizo
la nishati ambalo ndio pembejeo ya viwanda. Wakaweka sharti
kuwa fedha hizo na miradi hiyo itatekelezwa na Sekta Binafsi ya
Marekani.
Ndio sababu wengi wenu mtakumbuka hata Rais Obama alitangazia
dhamira ile pale Ubungo kwenye Mitambo ya Symbion Power na sio
kwamba alipenda kwenda kutembea Ubungo.
Kuanzia hapo kumekuwepo na shinikizo kubwa sana na masharti
magumu na yenye kuhamahama (shifting goal post) kutaka
kuibaka sekta ya nishati nchini ikiwemo mageuzi ya TANESCO.
Zikaainishwa hatua kadhaa,ambazo utekelezaji wake baadhi ni
kisheria na kisera na hivyo haziwezi kwenda kwa deadline
walizotaka.
Kila bodi ikikutana wanaibua hiki na kile lakini wakisema hela
watatoa. Hela hizi zikawa zimeshikiliwa kama chambo ukisogelea
zinasogea, ni sawa na ule mchoro wa Mpanda Punde aliyeshika
fimbo yenye majani na akiielekeza mbele ya punda, kwamba punda
ataendelea kuyafuata majani akidhani atayafikia kumbe ndio
anaupiga mwendo.
Hatimaye wakasema wanasubiri uchaguzi mkuu jambo ambalo
halihusiani na madai ya mwanzoni. Baada ya uchaguzi wakaibuka
na suala la Zanzibar.
Hivyo, uamuzi wao wa leo ni uamuzi uliotarajiwa. Pia ni uamuzi
wenye madhara kwa sekta binafsi ya Marekani pia ambayo ndio
ilikuwa itekeleze miradi hiyo.
Kama Taifa ni muhimu kulinda utu na uhuru wetu. Ndio msingi wa
sera yetu ya nje toka mwanzo na hata sasa. Tumetofautiana na
Marekani katika hili tutapatana katika mengine. Ndio uhai wa
maisha ya diplomasia.
Wao nao wanayo hadhira ya wapiga kura wao wanayojaribu
kuituliza huko nchini kwao kwa uamuzi huu. Tunapaswa
kuheshimu uamuzi wao kama ambavyo wanapaswa kuuheshimu
wetu.
Hatimaye baadae tutapatana. Marekani inaihitaji Tanzania zaidi na
Tanzania inaihitaji Marekani. Marekani inahitaji MCC 2 zaidi hali
kadhalika Tanzania inahitaji MCC 2.
Mahusiano ya Tanzania na Marekani hayakuanza na hayataisha na
MCC. MCC imeyakuta na itayaacha.
Kama marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ndio kigezo, basi Marekani
isingekuwa inatoa zaidi ya Dola Bilioni 3 kila mwaka kwa Egypt iliyo
chini ya utawala wa kijeshi kwa sababu ya kuununua ugomvi wa
Egypt na Israel na isingetoa kiasi cha dola bilioni 6 kwa Israel kila
mwaka kwa yale wanayoyafanya dhidi ya Wapalestina.
Huu ni wakati ambao Taifa linawaita Wazalendo wake. Wazalendo
wasimame na kusema 'Nchi yangu KWANZA, iwe Sahihi au
Imekosea" na Makuwadi watashangilia na kusema "si mnaona sasa
kiko wapi?".
Huu ni wakati wa kujifunga mikanda na kulinda heshima yetu kama
Taifa letu. Tuna vyanzo vya mapato vingi sana ambavyo
hatujaanza kukusanya mapato, tuwe wabunifu na tusibweteke na
kutegemea mapato yataongezeka maradufu kwa vyanzo vile vile.
Niseme kwa uchache, sababu walizotoa MCC, na ieleweke aliyetoa
tamko ni MCC, heri lingetoka tamko hili Wizara ya Mambo ya Nje au
Ikulu ya Marekani, moja ni Zanzibar na pili ni Sheria ya Makosa ya
Mitandao (Cyber crimes Act).
Sasa hebu tujadili kidogo, hivi kule Zanzibar tulitaka kitokee nini
pale ambapo wanasiasa walikuwa hawataki kujadiliana?
Tume ile ile ya Uchaguzi ambayo bado ilikuwa na uhalali wa kikatiba
na kisheria kuuitisha, kuufuta na kuuitisha tena uchaguzi ikachukua
nafasi yake.
Wanasiasa wasio makini wakaishia kuhamishia malumbano
mitandaoni badala ya kuitafuta suluhu ya kisiasa na pale siasa
iliposhindikana basi wangeitafuta suluhu katika mahakama za
Zanzibar.
Mezani wakashindwa, mahakamani hawakwenda. Tume ikachukua
uongozi, uchaguzi ukaitishwa Wananchi wakapiga kura na sasa
huko Zanzibar kuna serikali na baraza la wawakilishi.
Hata mimi sifurahii sana njia waliyoichukua Zanzibar lakini ilibidi
siasa za madaraka zisite ili tuanze kufanya siasa za maendeleo. Je
wamarekani walitaka muujiza gani utokee huko.?
Kuhusu Sheria ya Mitandao, hata mimi siipendi, si twende
mahakamani, bunge litaanza vikao muda si mrefu je wabunge si
wapeleke hoja ya kuifanyia marekebisho sheria hii.
Sasa Marekani (MCC) inapoweka shinikizo kwa suala la Sheria
ambayo ni jambo la ndani na linaloweza kujadilika, sijaelewa.
Mbona sie hatujapiga kelele Yule jamaa yao Trump alipotutusi
waafrika na kusema sisi stahili yetu ni kuwekwa tena chini ya
ukoloni (hapa nimechomekea tu).
INDHARI
Ni aibu kwa viongozi wa kisiasa kufurahia jambo hili, ni ishara ya
ukuwadi wa kisiasa na ambao uko tayari kukumbatia mahusiano
yanayotweza Uhuru wetu. It is now high time kufanya siasa safi za
maendeleo (politics of development) na sio kujikita katika katika
siasa za madaraka (Politics of Power).
*************
Imeandikwa  na: Humphrey Polepole.
Mwandishi, Ndg. Humphrey Polepole amenufaika na uelewa wa
watu wenye uzoefu wa mahusiano ya Tanzania na nchi za Nje.
Aidha, ni mnufaikaji (alumni) wa programu ya uongozi chini ya
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.