Tuesday, March 29, 2016

Uchambuzi wa Humphrey Polepole Kuhusu Marekani Kusitisha Msaada wa Mabilioni ya Pesa na Shughuli zake Tanzania

Nianze na nukuu hizi mbili kuntu za Baba wa Taifa Mwalimu Julius
K. Nyerere- Mwenyezi Mungu amrehemu.
“Democracy is not a bottle of Coca-Cola which you can import.
Democracy should develop according to that particular country”.
June 1991 in Rio De Janeiro, Brazil
"Demokrasia sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza.
Demokrasia lazima ikue na kuendelezwa kulingana na nchi husika".
Juni 1991 Rio De Janeiro, Brazil (Tafsiri ni yangu)
“No nation has the right to make decisions for another nation; no
people for another people”. From ‘A Peaceful New Year’ speech,
Tanzania, January 1968
"Hakuna Taifa lina haki ya kufanya maamuzi juu ya Taifa lingine;
wala watu juu ya watu wengine ". Hotuba ya Amani ya Mwaka
Mpya, Tanzania, Januari 1968 (Tafsiri ni yangu)
Hili la Marekani na uamuzi wa MCC ni jambo la mpito na haliwezi
kuua mahusiano yetu na Marekani. Tanzania na Marekani
zinashirikiana kwa mambo mengi na MCC ni sehemu tu tena ni
eneo jipya la ushirikiano.
Uamuzi huu ni jaribio kwa uhuru wa Taifa letu. Hakuna namna
nyingine ila kushinda hili kama tulivyoshinda mengine huko nyuma.
Kwa wale ambao wameuona umri watakumbuka namna tulivunja
uhusiano na Ujerumani Magharibi 1964 pale walipotaka kuwa na
kauli hasi dhidi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Tulivunja uhusiano na Ujerumani Magharibi baada ya kutaka
kuingilia Uhuru wa Mataifa Mawili huru yaliyoamua kuungana na
kuunda Nchi Mpya ambayo leo tunajivunia, Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
1965 Tulivunja uhusiano na Uingereza kufuatia na kitendo cha
wazungu wachache kujitangazia Uhuru (Unilateral Declaration of
Independence) kule Rhodesia na uingereza kukaa kimya na
kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Tulivunja Uhusiano na Uingereza kuieleza Dunia kwamba Uhuru wa
nchi za Afrika ni kipaumbele muhimu kwa Tanzania. Jambo
tunalopaswa kufahamu ni kuwa MCC 2 toka mwanzo imekuwa ni
mtihani dhidi ya uhuru wetu.
Napenda ieleweke kwamba kipindi hiki kilichotokea sio kuvunjika
kwa uhusiano wetu na Marekani bali taasisi ya MCC ndio imesitisha
msaada wao kwetu, lakini mahusiano yetu na marekani bado yako
pale pale, na si Marekani au Tanzania inayoweza kuugharimu
uhusiano wetu.
MCC 1 ilikuwa ni chambo cha kutuvuta na tulipewa bila masharti
tena hela nyingi dola milioni 698 na ni fedha tulizopewa moja kwa
moja na kupewa uhuru wa kuamua tuzitumieje.
Tanzania ilitakiwa kuainisha maeneo kisha wao wanatoa hela. Ndio
maana miradi kama ile barabara ambazo hazikuwa zikipata ufadhili
kwa kuwa hazikuonekana ni za kiuchumi na miradi ya maji ya
Morogoro na kwingineko iliingizwa humu na kupata ufadhili.
MCC 2 sio hivyo. Kwenye MCC 2 walengwa wakubwa ni sekta
binafsi ya Marekani, hapa kuna mtego hapa, hapa ni biashara hapa.
Mchakato wa MCC 2 ulipoanzishwa, wafanyabiashara kwa
kushirikiana na Maseneta wakaanzisha hoja kuwa kwanini
Marekani inatoa fedha kwa ufadhili katika nchi ambazo China ndio
wenye kufaidika na fedha hizo?
Wakaleta hoja ya kuwa Serikali ya Marekani ifanye jitihada ya
kuweka fedha kwa kusaidia Sekta Binafsi ya Marekani kupenya
Afrika.
Ukaitishwa mkutano wa US-Africa Summit na agenda kubwa ikawa
Power Africa. Katika Power Africa, Marekani ikalichagua eneo la
Nishati (si uzalishaji viwanda) kwa kutambua kuwa ndio eneo
pekee wanaloweza kushindana na wachina.
Wakasema wataelekeza fedha huko kuisaidia Afrika kutatua tatizo
la nishati ambalo ndio pembejeo ya viwanda. Wakaweka sharti
kuwa fedha hizo na miradi hiyo itatekelezwa na Sekta Binafsi ya
Marekani.
Ndio sababu wengi wenu mtakumbuka hata Rais Obama alitangazia
dhamira ile pale Ubungo kwenye Mitambo ya Symbion Power na sio
kwamba alipenda kwenda kutembea Ubungo.
Kuanzia hapo kumekuwepo na shinikizo kubwa sana na masharti
magumu na yenye kuhamahama (shifting goal post) kutaka
kuibaka sekta ya nishati nchini ikiwemo mageuzi ya TANESCO.
Zikaainishwa hatua kadhaa,ambazo utekelezaji wake baadhi ni
kisheria na kisera na hivyo haziwezi kwenda kwa deadline
walizotaka.
Kila bodi ikikutana wanaibua hiki na kile lakini wakisema hela
watatoa. Hela hizi zikawa zimeshikiliwa kama chambo ukisogelea
zinasogea, ni sawa na ule mchoro wa Mpanda Punde aliyeshika
fimbo yenye majani na akiielekeza mbele ya punda, kwamba punda
ataendelea kuyafuata majani akidhani atayafikia kumbe ndio
anaupiga mwendo.
Hatimaye wakasema wanasubiri uchaguzi mkuu jambo ambalo
halihusiani na madai ya mwanzoni. Baada ya uchaguzi wakaibuka
na suala la Zanzibar.
Hivyo, uamuzi wao wa leo ni uamuzi uliotarajiwa. Pia ni uamuzi
wenye madhara kwa sekta binafsi ya Marekani pia ambayo ndio
ilikuwa itekeleze miradi hiyo.
Kama Taifa ni muhimu kulinda utu na uhuru wetu. Ndio msingi wa
sera yetu ya nje toka mwanzo na hata sasa. Tumetofautiana na
Marekani katika hili tutapatana katika mengine. Ndio uhai wa
maisha ya diplomasia.
Wao nao wanayo hadhira ya wapiga kura wao wanayojaribu
kuituliza huko nchini kwao kwa uamuzi huu. Tunapaswa
kuheshimu uamuzi wao kama ambavyo wanapaswa kuuheshimu
wetu.
Hatimaye baadae tutapatana. Marekani inaihitaji Tanzania zaidi na
Tanzania inaihitaji Marekani. Marekani inahitaji MCC 2 zaidi hali
kadhalika Tanzania inahitaji MCC 2.
Mahusiano ya Tanzania na Marekani hayakuanza na hayataisha na
MCC. MCC imeyakuta na itayaacha.
Kama marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ndio kigezo, basi Marekani
isingekuwa inatoa zaidi ya Dola Bilioni 3 kila mwaka kwa Egypt iliyo
chini ya utawala wa kijeshi kwa sababu ya kuununua ugomvi wa
Egypt na Israel na isingetoa kiasi cha dola bilioni 6 kwa Israel kila
mwaka kwa yale wanayoyafanya dhidi ya Wapalestina.
Huu ni wakati ambao Taifa linawaita Wazalendo wake. Wazalendo
wasimame na kusema 'Nchi yangu KWANZA, iwe Sahihi au
Imekosea" na Makuwadi watashangilia na kusema "si mnaona sasa
kiko wapi?".
Huu ni wakati wa kujifunga mikanda na kulinda heshima yetu kama
Taifa letu. Tuna vyanzo vya mapato vingi sana ambavyo
hatujaanza kukusanya mapato, tuwe wabunifu na tusibweteke na
kutegemea mapato yataongezeka maradufu kwa vyanzo vile vile.
Niseme kwa uchache, sababu walizotoa MCC, na ieleweke aliyetoa
tamko ni MCC, heri lingetoka tamko hili Wizara ya Mambo ya Nje au
Ikulu ya Marekani, moja ni Zanzibar na pili ni Sheria ya Makosa ya
Mitandao (Cyber crimes Act).
Sasa hebu tujadili kidogo, hivi kule Zanzibar tulitaka kitokee nini
pale ambapo wanasiasa walikuwa hawataki kujadiliana?
Tume ile ile ya Uchaguzi ambayo bado ilikuwa na uhalali wa kikatiba
na kisheria kuuitisha, kuufuta na kuuitisha tena uchaguzi ikachukua
nafasi yake.
Wanasiasa wasio makini wakaishia kuhamishia malumbano
mitandaoni badala ya kuitafuta suluhu ya kisiasa na pale siasa
iliposhindikana basi wangeitafuta suluhu katika mahakama za
Zanzibar.
Mezani wakashindwa, mahakamani hawakwenda. Tume ikachukua
uongozi, uchaguzi ukaitishwa Wananchi wakapiga kura na sasa
huko Zanzibar kuna serikali na baraza la wawakilishi.
Hata mimi sifurahii sana njia waliyoichukua Zanzibar lakini ilibidi
siasa za madaraka zisite ili tuanze kufanya siasa za maendeleo. Je
wamarekani walitaka muujiza gani utokee huko.?
Kuhusu Sheria ya Mitandao, hata mimi siipendi, si twende
mahakamani, bunge litaanza vikao muda si mrefu je wabunge si
wapeleke hoja ya kuifanyia marekebisho sheria hii.
Sasa Marekani (MCC) inapoweka shinikizo kwa suala la Sheria
ambayo ni jambo la ndani na linaloweza kujadilika, sijaelewa.
Mbona sie hatujapiga kelele Yule jamaa yao Trump alipotutusi
waafrika na kusema sisi stahili yetu ni kuwekwa tena chini ya
ukoloni (hapa nimechomekea tu).
INDHARI
Ni aibu kwa viongozi wa kisiasa kufurahia jambo hili, ni ishara ya
ukuwadi wa kisiasa na ambao uko tayari kukumbatia mahusiano
yanayotweza Uhuru wetu. It is now high time kufanya siasa safi za
maendeleo (politics of development) na sio kujikita katika katika
siasa za madaraka (Politics of Power).
*************
Imeandikwa  na: Humphrey Polepole.
Mwandishi, Ndg. Humphrey Polepole amenufaika na uelewa wa
watu wenye uzoefu wa mahusiano ya Tanzania na nchi za Nje.
Aidha, ni mnufaikaji (alumni) wa programu ya uongozi chini ya
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

No comments:

Post a Comment