Wednesday, March 30, 2016

Japan yaikopesha Tanzania Bil 117

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati mbili za
makubaliano na Serikali ya Japan itakayoiwezesha Tanzania kupata
kiasi Yen Bilioni 6 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 117 za Kitanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini hati
hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius
Likwelile alisema mkataba wa kwanza utasaidia katika kukamilisha
bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17.
Dkt. Likwelile alisema kuwa msaada huo unalenga kuweka
mazingira rafiki kwa wafanyabiashara, kuboresha masoko na
kuwezesha mazingira ya ushindani katika utengenezaji wa ajira
nchini.
Mkataba wa pili unahusu masuala ya kiufundi yatakayotumika
katika kufanya marekebisho ya mkataba uliosainiwa Octoba 20,
1966, kwa kuzingatia sheria nyingi zimebadilika, kusainiwa kwa hati
hiyo ya makubaliano itasaidia kutabadilisha baadhi ya vifungu
vyenye jina Tanzania na kuweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ili kujumuisha pande zote mbili za Muungano katika kutekeleza
miradi ya maendeleo nchini.
Aidha, makubaliano hayo yatasaidia kubadilisha baadhi ya vipengele
vya mkataba uliopita ikiwemo kipengele cha usambazaji wa
madawa ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa ya wataalamu kutoka
nchini Japan kuweza kuja kufanya kazi za kujitolea hapa nchini
Tanzania.
Katibu Mkuu Dkt. Likwelile ameishukuru Serikali ya Japan na
kusisitiza kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa ili kuweza
kuwa na tija na kuwaletea maendeleo Watanzania.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida
amesema kuwa Serikali ya Japan ina imani kuwa ushirikiano uliopo
baina ya nchi hizi mbili utasaidia kukuza maendeleo ya uchumi na
kijamii.
Balozi Yoshida amesema kuwa Serikali ya Japani inaunga mkono
juhudi za Serikali inayo ongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika
masuala ya viwanda na mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji
kuwekeza nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment