Rais wa Sudan Omar al-Bashir amesema kwamba ataondoka
madarakani mwaka 2020 muhula wake wa sasa utakapomalizika
kwa mujibu wa BBC.
Bw Bashir pia amekanusha tuhuma kwamba wanajeshi wake
wamekuwa wakitekeleza dhuluma kwenye vita vipya dhidi ya
wanavijiji weusi katika eneo la Darfuf, magharibi mwa nchi hiyo.
Kiongozi huyo anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa
Kivita (ICC) kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na uhalifu
wa kivita.
Bw Bashir amekuwa madarakani tangu 1989. Alishinda uchaguzi
mkuu Aprili mwaka jana.
Bashir amesema kazi yake “inachosha” na kwamba muhula wake
wa sasa utakuwa wa mwisho.
“Mwaka 2020, kutakuwa na rais mpya na nitakuwa rais wa zamani,”
amesema.
Hata hivyo, wakosoaji wake watasema tayari amewahi kuahidi
kung'atuka awali lakini baadaye akakosa kutimiza ahadi hiyo.
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 2.5 milioni
wamefurushwa makwao Darfur tangu 2003, zaidi ya 100,000
wakitoroka makwao mwaka huu pekee.
Rais Bashir amesema hakuna haja ya kuwa na walinda Amani wa
Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa kutoa misaada eneo la Darfur.
Amekana taarifa za kutekelezwa kwa dhuluma zaidi maeneo ya
milima ya Jebel Marra ambapo wanajeshi wa serikali walianzisha
operesheni Januari.
"Madai haya yote hayana msingi, ripoti hizo zote hazina ukweli,”
amesema.
"Namtaka yeyote azuru vijiji vilivyotekwa na wanajeshi, na
wanioneshe kijiji kimoja ambacho kimeteketezwa.
"Kusema kweli, hakujakuwa na mashambulio yoyote ya kutoka
angani.”
Rais huyo amesema wote waliotoroka mapigano walikimbilia
maeneo yanayodhibitiwa na serikali na kwamba hiyo ni ishara tosha
kwamba serikali haiwashambulii raia.
Rais Bashir pia amesema makadirio ya UN kwamba zaidi ya watu
100,000 wametoroka makwao eneo la Darfur tangu Januari kwa
sababu ya mapigano “yametiwa chumvi na si ya kweli”.
Ni watu wachache sana ambao wametoroka makwao na
wamekimbilia maeneo yanayodhibitiwa na wanajeshi wa serikali au
maeneo ambayo yana wanajeshi wa kulinda amani wa UN, kikosi
ambacho hujulikana kama Unamid.
Amesema wanajeshi wa UN na walinda amani wa umoja huo
hawana jukumu kubwa la kutekeleza na wanafaa kuondoka nchini
humo.
Aidha, amesema mashirika ya kutoa misaada yanayotoa misaada
kwa wakazi eneo la Darfur hawana jukumu la kutekeleza kwa
sababu hakuna uhaba wa chakula Darfur.
Bw Bashir amesema makadirio ya Umoja wa Mataifa kwamba watu
2.5 milioni wanaishi kambini eneo la Darfur si ya kweli na kwamba
idadi ya kweli ni watu karibu 160,000.
Bw Bashir alipata asilimia 94 ya kura kwenye uchaguzi wa mwaka
jana ambao ulisusiwa na upinzani.
BBC
Thursday, April 7, 2016
Bashir atangaza kuachia ngazi 2020
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment